Mkoa wa Tanga ni mojawapo ya mikoa 31 ya Tanzania uliopo kaskazini-mashariki mwa nchi, ukiwa na makao makuu katika jiji la Tanga. Mkoa una eneo la km² 27,348 ambalo linaunganisha sehemu za pwani pamoja na milima. Unapakana na Mkoa wa Kilimanjaro upande wa kaskazini-magharibi, Mkoa wa Manyara upande wa magharibi, Mkoa wa Morogoro kusini-magharibi, na Mkoa wa Pwani upande wa kusini. Kwa upande wa mashariki, mkoa huu unapakana na Bahari ya Hindi, jambo linaloufanya kuwa na fursa nyingi za kiuchumi kupitia bandari, uvuvi, na utalii wa fukwe. Tanga ni miongoni mwa mikoa ya zamani zaidi nchini, ikiwa na historia tajiri ya biashara ya pwani na urithi wa Kiswahili. Uchumi wa mkoa unategemea kilimo cha mazao kama mkonge, biashara, na utalii unaotokana na vivutio kama Mapango ya Amboni, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, na Milima ya Usambara. Mwaka 2022 wakazi waliohesabiwa katika sensa walikuwa 2,615,597 kutoka 2,045,205 wa mwaka 2012.
Eneo la mkoa
Tanga ni kati ya mikoa midogo ya Tanzania ikiwa na msongamano mkubwa wa wakazi ndani ya eneo lake, hasa wilaya ya Lushoto kwenye ardhi yenye rutuba nzuri.
Eneo linalofaa kwa kilimo ni km² 17,000.
Kuna wilaya 11 ambazo ni Bumbuli, Handeni Vijijini, Handeni Mjini, Kilindi, Korogwe Vijijini, Korogwe Mjini, Lushoto, Mkinga, Muheza, Pangani na Tanga Mjini.
Hali ya hewa
Kwa jumla hali ya hewa ni joto lenye unyevu. Handeni kuna joto kavu zaidi. Milima ya Usambara hakuna joto sana.
Miezi ya Desemba - Machi halijoto huko Tanga inafikia sentigredi 30-32 mchana na 26-29 usiku. Wakati wa Mei hadi Oktoba halijota inapoa: ni sentigredi 23-28 mchana na 20-24 usiku. Unyevu iko juu kati ya asilimia 100 na asilimia 65.
Maeneo mengi ya mkoa hupokea angalau milimita 750 za mvua kwa mwaka au zaidi. Pwani ni zaidi: takriban milimita 1,100 hadi 1,400 ikipungua sehemu za ndani isipokuwa milima ya Usambara ambako mvua inaweza kuzidi milimita 2000 kwa mwaka.
Wakazi
Makabila makubwa mkoani Tanga ni Wasambaa, Wazigua, Wabondei na Wadigo. Mengine ni Wapare, Wataita, Wambugu, Wasegeju na Wanago. Pia kuna Waarabu wengiwengi wenye asili ya Oman.
Wasambaa ndio kabila kubwa lililoko katika milima ya Usambara, Muheza, Korogwe na Lushoto. Kwa jumla ndio asilimia 40 ya wakazi wote wa mkoa.
Wazigua ni kabila kubwa huko Handeni na sehemu za Korogwe na Pangani. Wabondei wako hasa Muheza na sehemu za Pangani. Wadigo ndio wengi Tanga yenyewe na sehemu za pwani.
Elimu
Uchumi

Wakazi wengi hutegemea kilimo cha riziki pamoja na ufugaji na uvuvi.
Mazao ya chakula hasa ni mahindi, muhogo, ndizi, maharagwe na mpunga.
- Mazao ya biashara ni katani, pamba, kahawa, chai, nazi, tumbaku na korosho.
- Mifugo ni ng'ombe, mbuzi na kondoo pamoja na kuku.
- Katani ilikuwa zao la biashara hasa kwa ajili ya Tanga tangu kuingizwa kutoka Mexico zamani za Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Hulimwa kote mkoani isipokuwa Lushoto, hasa Muheza na Korogwe kwenye mashamba makubwa. Mashamba hayo yalikuwa ya walowezi, yakataifishwa baada ya uhuru. Tangu kuanguka kwa sekta ya umma yamebinafsishwa tena siku hizi. Zao la katani linategemea sana soko la dunia, umuhimu wake ulirudi nyuma tangu miaka ya 1960.
Tanga ilikuwa na viwanda vingi kiasi katika miaka ya 1960 na 1970 lakini karibu vyote vimekwama kutokana na siasa ya Ujamaa na uchumi wake ulioiga mfumo wa nchi za kisoshalisti. Viwanda vichache vilivyobaki havizalishi mali kulingana na uwezo wao. Kilichobaki hasa ni kiwanda cha saruji Tanga.
Utalii umeanza kupanuka kidogo, hasa katika eneo la Pangani, Mapango ya Amboni na kituo cha Makumbusho Urithi Tanga.
Wilaya ya Handeni kuna machimbo ya madini.
Majimbo ya bunge
Wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015 mkoa huu ulikuwa na majimbo ya uchaguzi yafuatayo:
- Tanga Mjini: mbunge ni Ummy Mwalimu (CCM)
- Bumbuli: mbunge ni January Makamba (CCM)
- Mlalo: mbunge ni Rashid Abdakkag Shangazi (CCM)
- Pangani: mbunge ni Jumaa Hamidu Aweso (CCM)
- Kilindi: mbunge ni Omari Mohamed Kigua (CCM)
- Mkinga: mbunge ni Dustan Kitandula (CCM)
- Handeni Vijijini: mbunge ni Mboni Mohamed Mhita (CCM)
- Muheza: mbunge ni Hamis Mohammed Mwinjuma (CCM)
- Korogwe Mjini: mbunge ni Pius Kimea (CCM)
- Korogwe Vijijini: mbunge ni Stephen Hillary Ngonyani (CCM)
- Lushoto: mbunge ni
- Handeni Mjini: mbunge ni Omary Abdallah Kigoda (CCM)
Tazama pia
- Mkoa wa Tanga (DOA) - kuhusu mkoa wa zamani chini ya ukoloni wa Kijerumani
- Orodha ya milima ya mkoa wa Tanga
- Orodha ya mito ya mkoa wa Tanga
Viungo vya nje
- Tanga Region Socio-Economic Profile (Kiingereza)Ilihifadhiwa 10 Oktoba 2022 kwenye Wayback Machine. (PDF)
| Arusha | Dar es Salaam | Dodoma | Geita | Iringa | Kagera | Katavi | Kigoma | Kilimanjaro | Lindi | Manyara | Mara | Mbeya | Morogoro | Mtwara | Mwanza | Njombe | Pemba Kaskazini | Pemba Kusini | Pwani | Rukwa | Ruvuma | Shinyanga | Simiyu | Singida | Songwe | Tabora | Tanga | Unguja Kaskazini | Unguja Kusini | Unguja Mjini Magharibi | |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Tanga bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Mkoa wa Tanga kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.
